kabesejr blog

kabesejr

albino

Tuesday, May 14

YALIYOIBUKA BAADA YA BOMU ARUSHA HAYA HAPA


Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Arusha ambapo bomu lililipuliwa.
MUDA  mfupi tu baada ya bomu lilipotupwa na kulipuka kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Arusha, mambo mengi yakatawala. Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, moto ukawaka, huko yaliyozungumzwa ni chuki tupu za kidini.
Nianze kwa kuishauri serikali itunge sheria ya kudhibiti mitandao, maana inachipuka kama uyoga na jamii inatekwa. Huko kunazungumzwa mambo mazito, harakati nyingi haramu dhidi ya amani yetu, zinajadiliwa kwa uwazi. Ni hatari sana kwa mustakabali wa nchi yetu.
Haiwezekani kudhibiti bila kuwepo kwa sheria mahsusi. Katika sheria zinazosimamia vyombo vya habari, kwa upande wa mitandao ni bubu. Kama hatujui athari, basi tusome mapinduzi katika nchi za Libya, Misri, Tunisia, Algeria na kadhalika.

Hamasa yenye ujenzi wa chuki dhidi ya watawala, iliyoasisiwa na kustawishwa kupitia mitandao ya kijamii, ni kichocheo cha wananchi kusimama, wakaingia barabarani kisha wakafanya mapinduzi ambayo yaligharimu umwagaji damu. Watu wengi walipoteza maisha.
Hapa Afrika kuna nchi inaitwa Ivory Coast. Hii ilikuwa inasifika kwa amani na utulivu. Miaka ya nyuma iliigwa kama mfano. Baada ya chokochoko za kidini, wao wenyewe wakakubali kugawanyika, leo hii ile sifa waliyokuwa nayo imebaki simulizi na sasa wamegawanyika vipande vipande.
Ukienda Ivory Coast leo, unakuta watu wanaoitwa Ivorite (yaani wazawa) na wanaoitwa wageni ambao wazazi wao walienda nchini humo kufanya kazi miaka mingi. Kadhalika kuna mgawanyo wa kikanda ambao huu sasa chanzo chake ni udini.
Watu wa Kaskazini ni Waislam, wakati wale wa Kusini ni Wakristo. Mgawanyiko huo, ukasababisha kuundwa kwa Kundi la Muslim Burkinabis ambalo lilitaja dhamira yake kuwa ni kutetea Waislam. Hapo ndipo yakazuka mapigano makali, maafa ya kikatili yakatokea.
Mashambulizi mengi kutoka kwa dola na hata vikundi vingine vya raia wa kawaida, hususan Wakristo, yalielekezwa Kaskazini, hivyo Waislam wengi kuuawa. Hayo yalitokea kwa sababu raia wenyewe wa Ivory Coast waliamua kujigawa. Mpaka leo, chuki ya kidini bado ipo.
Wanajaribu, tena wanajitahidi sana kuhakikisha tofauti zao zinatoweka lakini hilo tayari ni doa. Chuki inaendelea na vita ya propaganda inastawishwa chini kwa chini. Leo hii, mtoto anayezaliwa Kaskazini, anakua akifundishwa kutambua kwamba wanaoishi Kusini ni maadui.
Kadhalika, wale wanaozaliwa Kusini wanaishi kwa muongozo wa kuwachukia Waislam wanaoishi Kaskazini. Wakati Ivory Coast wanaanzisha chokochoko za ubaguzi wa kidini, hawakujua kama hali ingekuwa mbaya kiasi hiki. Pengine hawakufikiria kuuana kikatili kiasi ambacho wamefikia.
Mtu anayethubutu kueneza chuki za kidini, hebu kwanza asome Ivory Coast ilikuwaje. Asiwe mzungumzaji bila kuwa na taarifa ya kile ambacho mataifa mengine walikivuna kutokana na harakati za kibaguzi ambazo walizianzisha. Hii ni nchi yetu, sisi wote ni ndugu, tuepuke chuki za kidini, ni mbaya sana.
Ipo Sierra Leone, ilikuwa nchi ambayo wageni walikuwa wanakarimiwa katika hali ambayo iliacha mshangao wa aina yake duniani. Ulimwengu mzima, hakukuwa na taifa linalothamini wageni na kuwapa huduma bora kama hilo la Afrika Magharibi. Uliza leo wapo wapi?
Sifa ya mshikamano, upendo na amani pamoja na ule utukufu wao wa kukarimu wageni havipo tena. Mapigano ya wao kwa wao ambayo moja ya sababu ni udini, yaliwafanya wageuke kutoka uzuri wa mfano wa malaika waliokuwa nao hadi kuwa waovu, wauaji mithili ya Shetani.
Sierra Leone ya leo ina rekodi kubwa sana ya kuwa na raia wenye ulemavu wa viungo mbalimbali vya mwili ambavyo walivipoteza wakati wa vita vya wao kwa wao. Watu wanaochochea tupigane, inaonekana hawajui na kama wanajua, basi dhamira yao ni katili kupitiliza.
Je, wanataka kuifanya Tanzania iwe Sierra Leone nyingine? Taifa liwe na walemavu kila kona, harufu ya damu inuke mikoa yote, watu wapoteane na familia zao, nchi yetu yenye amani itengeneze wakimbizi. Tafadhalini sana, tusikubali watu waigeuze Tanzania yetu sawa na Ivory Coast.
Kuhakikisha Tanzania haiwi Sierra Leone, hatuna budi kueneza neno la upendo badala ya chuki. Serikali isifanye mzaha, badala yake iamue leo kufuatilia na kushughulikia manung’uniko (grievances) kutoka kwenye makundi mbalimbali bila kujali dini zao.
Serikali ijue Waislam wanagawanyika kwa sababu zipi. Madai ya akina Sheikh Issa Ponda ni yapi. Iyashughulikie, vinginevyo ni kuzalisha maandamano na machafuko yasiyofaa katika sura ya taifa letu jema lenye amani. Kadhalika, kama kuna malalamiko ya Wakristo, ijulikane hoja yao ni ipi na ufumbuzi upatikane.
Tunapoishi kwenye jamii yenye makundi yanayonung’unika ni sawa na kuishi na bomu ambalo linapolipuka husababisha madhara makubwa sana. Hivyo basi, madaktari, walimu na wanafunzi, wasikilizwe malalamiko yao yashughulikiwe. Tusingoje athari, kinga ni bora kuliko tiba.
Tusikimbie ukweli kwamba tunaposhindwa kushughulikia madai ya hapa na pale, tunapopuuza manung’uniko yaliyopo kwenye makundi mbalimbali ya kijamii, tiba mahsusi inapokosekana, maana yake sasa tunakuwa tunajipanga kukabili vita. Sababu za mapinduzi ya Tunisia ni kielelezo cha mfano katika hoja hii.
Nchi yetu ni nzuri, Mungu wetu alivyotuchagulia hili ndilo liwe taifa letu, hakuweka ubaguzi wa kidini. Hii ndiyo sababu ya Waislam na Wakristo kuishi pamoja kama ndugu na majirani kila sehemu ya nchi yetu. Laiti tungejifunza hali halisi ya udini Nigeria, pengine tungeheshimu na kuenzi amani na utamaduni wetu wa Waislam na Wakristo kushirikiana.
Nigeria ilivyo, kiasili imegawanywa kidini. Hii ndiyo sababu tofauti za hapa na pale hujiri na kuitikisa nchi hiyo. Unapokuwa Kaskazini, kule Waislam wametawala, vilevile wapo Kusini Magharibi ya nchi hiyo. Kabila la Yoruba ndilo lenye Waislam wengi, wakati Kabila la Igbo wengi wao ni Wakatoliki.
Hapo utaona jinsi walivyogawanyika. Yaani ukipiga Waigbo, unawapiga Wakatoliki kwa wakati mmoja. Tanzania yetu, sisi sote ndugu. Tulivyo ni sawa na familia moja. Sasa basi, ili kuendelea kuishi kwa upendo ni lazima tukatae na tuwakemee wote wanaotaka kutugawa.
Kama kuna uwakala uliopandikizwa ili kuifanya nchi isambaratike, tuukatae. Maana watapiga mabomu Kanisa ili kuwafanya Wakristo waamini wanapigwa na Waislam au watavunja Msikiti halafu Waislam waseme maadui zao ni Wakristo.
Sasa basi, Ivory Coast, Sierra Leone, Nigeria na nchi nyingine, ziwe mfano kwetu. Serikali itimize wajibu wake, viongozi wa kidini wawausie waumini wao wote kupendana, Waislam wapendane na Wakristo, vilevile Wakristo wapendane na Waislam. Mimi nawapenda Waislam na Wakristo, wote ni ndugu zangu, nawe iambie nafsi yako itamke hivyo. Hakika sisi Watanzania tunapendana, hakuna udini wala uadui kati yetu.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...