kabesejr blog

kabesejr

albino

Thursday, May 24

WANAFUNZI WA UDSM WAUZA MIILI KUKIDHI HAJA ZAO




KAMATI ya Bunge ya masuala ya Ukimwi imeelezwa kwamba ukosefu wa mikopo na uhaba wa mabweni ,unasababisha baadhi ya wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wauze miili yao na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa Ukimwi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Rosweeter Kasikila kukutana na Uongozi wa Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam na Mzumbe ili kujionea hali ya Ukimwi katika vyuo hivyo.

Waziri wa Afya na Chakula wa Serikali ya wanafunzi wa UDSM, Cosmas Nzowa aliiambia kamati hiyo jana jijini Dar es Salaam kwamba , wanafunzi wengi wanaonekana kwenye sehemu za starehe wakijiuza kwa sababu wameshindwa kuendesha maisha yao.

“Wamefika chuoni wakitokea mikoani wakakuta hakuna mikopo wala mabweni ya kulala na hawana ndugu hapa jijini, unategemea wafanye nini, sasa wengi wanajiuza ili kujikimu, ukitembelea sehemu nyingi za starehe utawakuta,” alisema Nzowa.

Alisema , mchana wanakwenda chuoni lakini usiku wanakuwa na shughuli nyingine za kujiongezea mapato.
Aliongeza kuwa hata wanafunzi wanaume wanapokosa mikopo na mabweni ya kulala vyuoni huwa katika wakati mgumu na kulazimika kuishi na wanawake waliowazidi umri huko mitaani.

“ Sasa huku hatufahamu kama wanafunzi hawa watakuwa salama katika maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwani ni jambo la kawaida kukuta kijana mdogo wa chuo kikuu akiishi na shugamami mtaani,” alisema Nzowa.

Alisema ili kurekebisha hali hiyo utaratibu wa utoaji wa mikopo hauna budi kubadilishwa ili wanafunzi kabla hawajafika chuoni wawe wanafahamu kama watapata mikopo au la.
Aliongeza kuwa ,serikali iweke kipaumbele kwa kuongeza idadi ya mabweni inayolingana na wanachuo 15,000 waliopo hivi sasa.

“ Ili kuwasaidia wenzetu ambao wamekosa maeneo ya kuishi na hawana fedha, inabidi tuishi watu wanne kwenye vyumba vidogo na hivyo kusoma katika mazingira magumu,” alisema Nzowa anayesomea Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Jamii na Kiswahili.

Aliwaambia wabunge hao kwamba, wanafunzi hao wako katika hatari ya kupata maambukizo ya virusi vya ukimwi kutokana na mazingira magumu wanayoishi.

“Tunaiomba kamati hii itutembelee chuoni ili isikilize kilio cha wanafunzi hao,”alisema.
Mratibu wa Ukimwi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo aliieleza kamati hiyo kwamba, maambukizo katika chuo hicho baada ya kupima mwaka 2011 ni asilimia 2.3.

Makamu Mwenyekiti wa kamati, Kasikila alitaka uongozi wa chuo hicho kuwasilisha mbele ya kamati hiyo taarifa yenye kueleza matatizo mbalimbali yanayokwamisha mapambano dhidi ya Ukimwi chuoni hapo.
“Tukipata taarifa yenye changamoto mbalimbali itawasaidia wabunge kutetea Bungeni hasa katika suala zima za upatikanaji wa fedha za shughuli za Ukimwi,” alisema Kisikila.

Akichangia, Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim alisema mavazi wanayovaa wanafunzi wa UDSM yanahamasisha ngono.

“ Wanafunzi wa kike katika chuo hiki hawatofautishi mavazi ya disko na ya darasani, wanatembea nusu uchi hebu jifunzeni kwa wenzenu wa Chuo cha Biashara (CBE) wamedhibiti hilo,” alisema.Naye Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani alisema matatizo ya kifedha ya wanafunzi wa vyuo vikuu yanaweza kuwa kuwa kichocheo cha maambukizi ya Ukimwi.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...