![]() |
Kikosi cha Azam |
AZAM
leo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ili kuuzoea kabla
ya kushuka dimbani kesho kumenyana na wenyeji, Kagera Sugar kwenye
Uwanja huo huo ‘mbovu ile mbaya’ katika mchezo wa awali wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Azam
jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa seminari ya Mtungamo na zaidi
wachezaji walikuwa wanalalamikia baridi kali, tofauti na hali ya joto
waliyoizoea Dar es Salaam.
Mshambuliaji
wa zamani wa Kagera Sugar, Philipo Alando, ambaye kwa sasa ni mmoja wa
viongozi wa klabu hiyo ya Chamazi, ndiye ameongoza msafara wa timu
Bukoba, kwa yeye ni mwenyeji huko, lakini pia John Bocco, Luckson
Kakolaki na Gaudence Mwaikimba si wageni huko.
Alando
ambaye alistaafu soka akiwa na jezi ya Azam miaka miwili iliyopita,
amepewa jukumu la kuhakikisha anaiongoza Azam kubeba pointi sita za
mwanzoni za Ligi Kuu katika mechi mbili za Kanda ya Ziwa, baada ya mechi
ya keshokutwa watakwenda Mwanza, kuivaa Toto African.
Kocha
Mkuu wa Azam FC, Mserbia Boris Bunjak amesema timu yake ipo tayari kwa
Ligi Kuu, lakini tu amehadharisha marefa wachezeshe kwa haki.
Bunjak
alikerwa mno na marefa waliochezesha mechi ya Ngao ya Jamii Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam juzi kwamba waliwabeba wapinzani wao Simba SC.
Mechi
hiyo ilichezeshwa na Martin Sanya, aliyeisaidiwa na Omar Kambangwa na
Ephron Ndissa, wakati refa wa akiba alikuwa Oden Mbaga na Kamisaa Omary
Kasinde.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada
ya mechi hiyo, Bunjak alisema kwamba marefa hao walionyesha mapungufu
makubwa kwa kuwapendelea wazi wazi Simba na hata wakafanikiwa kutoka
nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
“Nafikiri
tulicheza mechi nzuri, tukaongoza 2-0, baada ya hapo tukapoteza nafasi
nzuri za kufunga, lakini siamini kwa nini refa alitoa penalti dakika ya
mwisho(kipindi cha kwanza), kwa sababu ule mpira ulikuwa kwenye himaya
ya wachezaji watatu kutoka nyuma, unaweza kuonaje nani aliucheza kwa
mkono.
Bao
la pili pia, pia ulikuwa msaada mkubwa, niliandaa timu yangu kucheza
dhidi ya wachezaji 10, siyo wachezaji zaidi, mimi si kocha nayeandaa
timu kucheza dhidi ya wachezaji wengi, naweza kufanya nini, tulicheza
vizuri, tulipoteza nafasi, refa alitunyima penalti mbili, asilimia 100,
naweza kufanya nini, labda hii ni soka ya Tanzania tu.
Nitafanya
nini, huu ni uzoefu wangu wa kwanza ofisini tena, lakini
nimeshashangazwa sana, Simba ni timu kubwa, Simba ni timu nzuri, lakini
leo Azam imecheza vizuri, Azam ilistahili kushinda taji,”alisema.
Kocha
huyo alionyeshwa kuridhishwa na bao moja moja tu la Simba, la tatu
ambalo alisita kulizungumzia kabisa katika malalamiko yake.
Azam
juzi iliiruhusu Simba SC kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2,
hivyo kutwaa Ngao ya Jamii, kwa mara ya pili mfululizo Uwanja wa Taifa,
Dar e s Salaam.
Shujaa
wa Simba jana alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la
ushindi dakika ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa
wa Azam, Deo Munishi ‘Dida’ amekaaje.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na
John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa
namba moja Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco
alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa
kona fupi na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud
ambaye alimrudishia mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa
nyavuni pembezoni mwa lango kulia.
Bocco
ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC leo,
alimtoka Amir Maftah upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya
kutoa krosi fupi kwa Kipre aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la
pili dakika ya 35.
Simba
ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada
ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo
kwa penalti, baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi
cha pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira
ya pembeni, ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa
wakibadilishana reli.
Kwa
staili hiyo, haikushangaza Simba ilipotumia dakika 45 za mwisho kwa
kufunga mabao mawili yaliyowatoa nyuma kwa 2-1 na kuibuka kidedea kwa
ushindi wa 3-2.
Emanuel
Okwi alimchambua kama karanga Erasto Nyoni na kuingia ndani kabisa
akiwatoka mabeki wengine wa Azam, kabla ya kuujaza mpira nyavuni kwa
shuti kali na Kazimoto akamaliza kazi dakika ya 78.
Kwa
ujumla katika mchezo huo, Azam ilitawala kipindi cha kwanza na ilikosa
mabao mawili zaidi ya wazi kupitia kwa Himid Mao na Kipre, lakini
kipindi cha pili Simba walitawala mchezo na kama wangekuwa makini, nao
wangeweza kuvuna mabao zaidi.
Naibu
Waziri wa Kazi, Makongoro Mahanga alimkabidhi ngao Nahodha wa Simba,
Juma Kaseja baada ya mechi hiyo, ambaye alikwenda kushangilia na
wachezaji wenzake na mashabiki wa timu hiyo.
No comments:
Post a Comment