Magari ya jeshi yakiwa yamezuiwa barabarani baada ya wanajeshi kumshambulia trafiki. (Picha na Mjengwa Blog)
MWAKA 1979 Idd Amin anaishambulia Tanzania. Nyerere anatangaza vita,
wote tunakubali kupambana naye. Mimi na polisi wenzangu tunapelekwa
vitani tena mstari wa mbele. Huko tunakutana na wanajeshi, mgambo na
makundi mengine mbalimbali. Tumepambana mpaka mwisho. Tumeshiriki vita
Comoro, na nchi nyingine mbalimbali ambazo zilihitaji huduma za kijeshi.
Huko hakukuwa na cha Mwanajeshi au polisi, wote thamani yao ilikuwa
sawa. Naenda Darfur Sudan, huko nakuta polisi ana thamani kubwa tena
analipwa vizuri kuliko Mwanajeshi. Yaonekana UN wanajua thamani ya
polisi katika jamii.Leo narudi Tanzania nakutana na kitu cha ajabu sana ambacho kinanifanya nishangae kweli kweli. Eti Traffic Officer ambaye anaaminiwa kutawala makutano ya barabara ya Morogoro na Mandela anapigwa makofi saa 10:15hrs asubuhi, mbele ya hadhara/kadamnasi ya wapita njia, madereva na wafanyabiashara ndogondogo. Anayefanya hivyo ni mwanajeshi. Ukitafuta sababu eti amewachelewesha wao watu muhimu wanaotoka Mwenge kwenda kambini kwao Twalipo Temeke. Ni wakurugenzi wangapi wanasimama barabarani kutii amri ya Traffic, ni mabalozi wangapi wanasimama barabarani kufuata maelekezo ya Traffic, ni mara ngapi msafara wa Rais unashindwa kuanza safari zake mpaka Traffic anapotoa taarifa kuwa barabara ni salama, ni mara ngapi hata IGP anasimama barabarani kwenye foleni hadi aombe msaada wa kupitishwa iwapo kuna dharura. Lakini leo mwanajeshi ambaye amepitia mafunzo ya paredi tu, anamdhalilisha afisa wa polisi.
Niambieni wapiganaji wenzangu, katika jamii tunayoishi leo, nani muhimu kati ya jeshi la polisi na Jeshi la Wananchi? Natoa masaa sita wanajeshi wagome wasifanye kazi yoyote, walale nyumbani, kambi zao wafunge - Je, kuna madhara gani kwa mwananchi, mwanakijiji wa kule Mtangimbole Songea, au Nyantira kule Musoma? Baada ya wao kumaliza masaa yao sita, nawakaribisha Polisi pia nao wagome kwa masaa sita - Wafunge vituo vyao vya polisi. Niambie ni akina mama wangapi watabakwa, ni vibaka wangapi watavamia maduka na makazi ya watu, ni benki ngapi hazitakuwa salama, msongamano wa magari utakuwaje, Je, kuna mtu ataenda kazini, kuna uzalishaji mali utafanyika? Lakini hili haliwezi kuonekana kwa leo, vinginevyo uwe na "Philosophical view".
Namkumbuka mbunge mmoja wa kaskazini ambaye ameomba nisimtaje jina alipokuwa anachangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Yeye alitoa angalizo kwa kusema, " Tabia ya kuweka tofauti katika maslahi kati ya Wanajeshi na Polisi, kiasi cha wengine kulipwa mshahara mara mbili au tatu ya ule wa mwenzake wa cheo kile kile, ni kukaribisha mgawanyiko wa wengine kujiona bora kuliko wenzao". Haya ndiyo yale yaliyotokea jana pale Ubungo. Mwanajeshi kwa kuwa analipwa tofauti, anamwona polisi sawa na mgambo. Nimejisikia fedheha kwa sababu sio mara ya kwanza, au ya pili, au ya tatu. Mwanajeshi kuvamia kituo kumchukua mwenzao ambaye ni mtuhumiwa si kitu cha ajabu. Polisi tupo kimya. Hii dharau itaisha lini. Je, wanataka tufanye nini ili tupate heshima tunayostahili?. Tugome; HAPANA, Tuvamie kambi za jeshi; HAPANA, Tuondoe mahusiano yaliyopo kati yetu na wao; HAPANA, Nifanye nini sasa?