Rais wa TFF, Leodegar Chillah Tenga atatetea nafasi yake? |
RAIS wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga atatetea nafasi yake
katika uchaguzi ujao wa shirikisho hilo, Desemba mwaka huu.
Habari
ambazo KABESEjr imezipata kutoka kwa watu walio karibu na Tenga,
zinasema kwamba awali beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliamua
kutogombea, lakini baada ya kushawishiwa na swahiba wake, rais wa Shirikisho la
Soka la KImataifa (FIFA), Sepp Blatter sasa atagombea.
“Tenga
atagombea tena TFF, unajua Blatter ni rafiki yake na ndiye amemuomba aendelee,
na Blatter mwenyewe atakuja hapa kumfanyia kampeni Tenga,”alisema mtu mmoja wa
karibu na Tenga.
Taarifa zaidi
zinasema tayari Tenga amekwishaanza kuwasiliana na wapiga kura na magwiji wa
kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Juhudi za
kumpata Tenga mwenyewe kuzungumzia habari hizo hazikufanikiwa, lakini kama
atagombea maana yake atachuana na Makamu wake wa sasa, Athumani Nyamlani ambaye
kwa muda mrefu inaelezwa amekwishaanza kampeni.
Upinzani
zaidi kwa Tenga iwapo kweli atagombea unatarajiwa kutoka kwa Jamal Emil
Malinzi, aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi uliopita Desemba 14, mwaka
2008.
Katika uchaguzi
huo, Tenga alitetea nafasi yake kwa kumbwaga Malinzi kwenye ukumbi wa NSSF
Waterfront kwa kura 64 dhidi ya kura 39 za Malinzi.
Awali
Malinzi alienguliwa kwa kigezo cha uzoefu, lakini akarejeshwa kuwania nafasi
hiyo baada ya kushinda rufaa yake.
Katika
uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mwakilishi wa FIFA, Ashford Mamelodi, Athumani
Nyamlani alishinda nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, baada ya kujikusanyia
kura 65 kati ya kura 107 zilizopigwa na kura mbili kuharibika, akimshinda Lawrence
Mwalusako aliyepata kura 39 na Ali Mwanakatwe aliyeambulia kura moja.
Nafasi ya
Makamu wa Pili wa Rais, ilikwenda kwa Ramadhani Nassib aliyemwangusha mpinzani
wake wa karibu, Damas Ndumbaro aliyepata kura 45.
Baadhi ya
wagombea wanaotajwa kuwania nafasi ya Makamu wa kwanza wa rais katika uchaguzi
ujao ni Frederick Mwakalebela, Wallace Karia, Michael Wambura, Wakili Alex Mgongolwa,
Wakili Imani Madega, Wakili Damas Ndumbaro na Lawrcence Mwalusako.
No comments:
Post a Comment