|
Girish Khetia wa Bidco Oil Limited (kulia), akimvalisha Shauri mkanda wa ubingwa wa IBF Afrika, baada ya kumpiga Kizito (kulia) |
BONDIA Ramadhan Shauri wa Tanzania, usiku huu amefanikiwa kutwaa
ubingwa wa Afrika wa Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF), baada ya kumpiga
kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya nane, Sunday Kizito wa Uganda katika
pambano lililokuwa la raundi 12, ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Baada ya kuokolewa kwa kengele kufuatia kipigo kikali kuanzia raundi
ya saba, Kizito aliporejea kwenye kona yake ya bluu, alifikia kuangukia magoti,
akishindwa kujimudu hadi aliposaidiwa na wasaidizi wake ambao walimuinua mikono
juu kuashiria hawezi kuendelea na pambano.
Awali, Kizito alionyesha upinzani mkali kwa Mtanzania huyo kuanzia
raundi ya kwanza hadi ya nne, lakini taratibu mambo yalianza kumgeukia kuanzia
raundi ya tano. Mikono miepesi ya Shauri iliyokuwa ikichomoka kwa haraka na
kutua kwenye kichwa cha Kizito, ilikwenda ikimlainisha taratibu Mganda huyo na
kufikia raundi ya nane, haikuwa ajabu alipotandikwa kama begi.
Shauri alipigana kwa kiwango cha juu na kuashiria kwamba, taifa limempata
shujaa mpya wa ndondi wa uzito wa Feather ambaye anaweza kufanya makubwa, kama
atapewa sapoti ya kutosha.
Pambano hilo liloandaliwa na Kitwe Promotions na kudhaminiwa na Bidco
Oil Limited, chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC)
lilitanguliwa na mapambano mengine kadhaa na Mtanzania mwingine, Nassib Ramadhan
alimpiga kwa TKO raundi ya kwanza, dakika ya kwanza sekunde ya 40, Mkenya Isaac
Odhiambo katika pambano la uzito wa Super Fly, lililokuwa la raundi nane.
Ramadhani Mashudu alimpiga Ramadhani Mkundi kwa pointi za majaji wote
watatu, katika pambano la raundi sita uzito wa Bantam, wakati Yonas Segere
alimpiga kwa pointi za majaji wawili kwa mmoja, Seba Temba katika uzito wa
Super Light, raundi sita pia na Bakari Mohamed alimpiga Bakari Maulid kwa
pointi za majaji wawili kwa mmoja, uzito wa Feather, raundi nne.
Kwenye ukumbi wa Chuo cha Uhasibu, Kurasini, lilifanyika pambano lingine
la uzito juu na Alphonce Mchumia Tumbo alimtandika TKO, raundi ya kwanza,
dakika ya kwanza sekunde ua 49, David Mrope ‘Zola D’.
|
Meza kuu |
|
Bondia Mada Maugo kulia akiwa na mwanamuziki Lady Maureen kutoka Kenya |
|
Girish Khetia kulia na Rais wa TPBC, Onesmo Ngowi |
|
Yonas Segere kushoto na Seba Temba |
|
Ramadhani Mashudu kushoto na Ramadhani Mkundi |
|
Ramadhani Mashudu kushoto na Ramadhan Mkundi |
|
Nassib Ramadhani kulia na Isaac Odhiambo |
|
Odhiambo akijikusanya kuinuka baada ya kukalishwa chini na konde la Nassib |
|
Promota Rutta wa Kitwe kushoto na Khetia |
|
Jaji Boniphace Wambura |
|
Shauri kushoto |
No comments:
Post a Comment