KUTOKANA na kutokea kwa ajali ya meli ya MV Skagit ambayo imezama juzi, wachezaji wa Yanga na Azam FC wameelezea jinsi ajali hiyo ilivyowagusa.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo wa Azam, Abdulhalim Humud wameweka wazi kuwa wamesikitishwa na ajali hiyo, ambapo wametoa msisitizo kwa serikali kuwa makini na masuala ya vyombo vya usafiri wa majini.
“Huu ni msiba mkubwa kwetu, kwani ni mara ya nne sasa hali kama hii inatokea, watu wengi wanapoteza maisha katika ajali mbaya kama hii, serikali inatakiwa iwe makini kuangalia chanzo cha tatizo, pia usafiri wa vyombo husika unatakiwa ufanywe kwa kiwango cha juu,” alisema Humud.
Cannavaro alisema: “Tukio kama hili linasikitisha sana kwani hii ni mara ya pili meli kuzama na kuua watu wengu, tuna ndugu zetu wengi ambao tumewapoteza katika ajali hiyo, inatuuma sana.”
Wakati huohuo Chama cha Soka Zanzibar(ZFA) kimesitisha masuala yote ya michezo kutokana na msiba huo mkubwa uliosababisha zaidi ya watu 30 kupoteza maisha, kauli ambayo ilitolewa na Makamu wa Rais wa ZFA, Ali Mohamed Ali.
Upande wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), kupitia Ofisa Habari, Boniface Wambura alisema mechi za jana za michuano ya Kombe la Kagame zilitarajiwa kuchezwa huku wachezaji wa timu zote wakivaa vitambaa vyeusi ili kuomboleza.
Source globalpublishers.com
No comments:
Post a Comment