kabesejr blog

kabesejr

albino

Friday, May 18

BOBAN AJA TCC PEKU PEKU, AMLILIA PATRICK MAFISANGO SANA



MSIBA wa aliyekuwa mchezaji wa Wekundu wa Msimbazi Simba Patric Mutesa Mafisango umewagusa mamia ya watu hapa nchini na hasa wapenzi wa soka na wachezaji kwa ujumla huku ukimgusa zaidi mchezaji mwenzake Haruna Moshi ‘Boban’ na kupelekea jana kutinga Sigara ambapo mwili wa marehemu ulikuwa ukiagwa bila ya kuwa na kiatu mguuni.

Mara baada ya wachezaji wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambao wako kambini katika hotel ya Tansoma kwa ajili ya kujiwinda na mechi ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 kwa kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast kufika katika viwanja hivyo wakiwa wanashuka katika basi ndipo Boban alishikwa na butwaa mara baada ya kujina yuko peku.

Aidha Boban licha ya kuwa peku alijikuta amepanda katika basi hilo huku akiwa hajapiga mswaki wala kunawa uso ambapo ilipelekea mmoja wa viongozi wa Stars kutoka uwanjani hapo na kwenda kumnunulia ndala na mswaki.

Boban alipoulizwa na mmoja wa viongozi kulikoni hata hajavaa viatu wala kunawa uso alibaki akimtazama huku akijiangalia bila ya kuamini kama ni kweli ameweza kufika katika eneo hilo bila ya kuwa na kiatu mguuni.

Kiongozi mwingine wa Stars alifanya jitihada za kuwa nae karibu nyota huyo mpaka kiongozi mwenzake alipoleta Mswaki na kandambili za bluu ambazo Baban alizivaa mpaka mwisho wa shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa rafiki yake wa karibu na mcheziji mwezake katika timu.

Aidha Boban kutokana na machungu ambayo alikuwa nayo alishindwa kuvumilia kukaa katika eneo ambalo timu ya Stars ilikuwa imepangiwa kukaa na kunyanyuka na kwenda kukaa chini karibu na jeneza la aliyekuwa rafiki yake marehemu Mafisango na kuwafanya watu mbalimbali waliofika katika eneo hilo kuangua vilio.

Mara baada ya Boban kutinga uwanjani hapo bila ya kiatu mguuni mwandishi wa habari hizi alimfuata mmoja wa viongozi wa Stars ambaye alisema kuwa licha ya kufika hapo bila ya viatu ilikuwa wamuache kambini kwa kuwa mara baada ya kupanda kwenye gari walishangaa hawamuoni na kurudi vyumbani na kumkuta amelala usingizi kutokana na uchovu mara baada ya juzi kushinda msibani.

Kifo cha Mafisango kimepelekea Stars Kushindwa kufanya mazoezi siku ya jana asubuhi na kupelekea kufanya mazoezi jioni kwa kuwa wachezaji wote walitinga Sigara kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.














No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...