MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake jioni hii ofisini kwake, jengo la NSSF, barabara ya Bibi Biti, Dar es Salaam, siku moja baada ya kuvamiwa na kundi la watu nyumbani kwake, Mbezi, Jijini usiku wa wa manane.
Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa jana na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee.
Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
"Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema
TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:
LLOYD NCHUNGA
BIHARAGU
C/O LLOYD
ADVOCATES,
Morogoro/Bibi
TIti Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension
towers
P.BOX 75111,
Dar-Es- Salaam,Tanzania.
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA
YANGA.
Ndugu wana Habari, najua
kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa
ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita
kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao
tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu
linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa
kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba
tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale
tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote
tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani
tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja,
yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa
wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja
kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya
tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa
katika klab yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana
mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium
Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa
wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata
hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua
za mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia
mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya
marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni
ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya
promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na
kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya
shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka
mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa
yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua
tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa
sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi
ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika
kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha
miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa,
na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika
Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo
maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni
kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki
ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo
tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu
Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali
Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika
suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili
mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali,
tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata
baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa
na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti
wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea
hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI
MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na
sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza
kuubaini mapema.
Sioni mantiki katika hoja
kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu
alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi
kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na
baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na
wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji
walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa
kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha,
kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa
uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi
kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao ,
Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu
hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko
mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA
MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto
naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme
amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua
kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda
hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba
yetu.
Vile vile siko tayari kuona
klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni
kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji
kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja
na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa
mafanikio zaidi.
Nitaendelea kuwa mwanachama
mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na
nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA
MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA
BIHARAGU.
Nakala
kwa:-
Mama Fatma
Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa
taarifa
No comments:
Post a Comment