Simba SC |
SUDAN
iko hatarini kufungiwa kucheza michuano ya klabu Afrika, kutokana na malalamiko
ya timu mbili, Simba SC ya Tanzania na TP Mazembe ya DRC kutumwa Shirikisho la
Soka Afrika (CAF) dhidi ya vitendo vya kihuni na visivyo vya kiunamichezo
ambavyo klabu hizo zimefanyiwa nchini humo.
Simba
SC imetuma malalamiko Afrika (CAF) leo kutokana na vitendo visivyo vya
kiuanamichezo inavyofanyiwa nchini Sudan inakosubiri pambano lake dhidi ya Al
Ahly Shendy kesho.
Taarifa
ya Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamgwa kutoka Sudan, imesema kwamba tangu wawasili
nchini Sudan juzi, wamekuwa ikifanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wenyeji
wake, Shirikisho la Soka Sudan (SAF) na Al Ahly Shendi.
Jana,
Simba ilifanyiwa vitendo hivyo kabla ya kwenda katika mji wa Shendi
itakakochezwa mechi hiyo na baada ya kufika katika mji huo uliopo takribani
kilomita 170 kutoka mji mkuu Khartoum.
Simba
iliwasili Shendi majira ya saa mbili usiku kwa saa za Sudan (sawa na saa za
huko) baada ya safari ya takribani masaa manne kutoka Khartoum.
Safari
ya kutoka Khartoum hadi Shendi ilianza majira ya saa kumi jioni na timu ikafika
saa mbili usiku, kwa maana ya masaa manne ya safari ya barabara jambo ambalo ni
kinyume cha kanuni za CAF zinazozungumzia umbali usiozidi masaa
mawili.
Ingawa
kanuni ya CAF kifungu cha 5 (3) kinazungumzia umbali wa kusafiri kwa basi
usizidi kilomita 200, Simba inaweza kutuma malalamiko kwamba kutoka Khartoum
hadi Shendi ni zaidi ya kilomita 150 kwa vile si haiwezekani kutumia masaa manne
kwa umbali huo.
Zaidi
ya usumbufu huo wa kusafiri muda mrefu, Simba pia inajiandaa kutuma malalamiko
CAF kwa vile hoteli waliyopangiwa haina kiwango kinachokubalika na shirikisho
hilo.
Kwa
mujibu wa kanuni ya CAF kifungu cha 7 (c), timu mwenyeji inatakiwa kuhakikisha
kuwa timu mgeni inaishi katika hoteli ya daraja la kwanza na pia msafara mzima
unakaa katika hoteli moja.
Hata
hivyo, Simba imewekwa katika hosteli inayofanana na mabweni ya wanafunzi na
imepewa vitanda 24 tu huku msafara ukiwa na watu takribani 30.
Wakati
ilipokuja Tanzania, Simba ililipia gharama za watu 30 wa timu hiyo na kulikuwa
na makubaliano kwamba na wao watafanya hivyo wakati Wekundu watakapokwenda
Sudan.
Kutokana
na ukosefu huo wa vyumba, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alilala kwenye
makochi ya chumba cha mapokezi pamoja na kocha msaidizi wa makipa wa Simba,
James Stephan Kisaka. Viongozi wengine wa Simba, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji,
Swedy Mkwabi na kiongozi wa msafara, Hussein Mwamba ambaye ni mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya TFF, pia walikosa pa kulala na hivyo wakalazimika kwenda kulala
nje ya hosteli hiyo ya Shendi.
Wakizungumzia
hali hiyo, wawakilishi wa timu ya Shendi walidai kwamba inatokana na ukweli kuwa
mji wao ni mdogo na hakuna hoteli nyingine kubwa kuliko hiyo mji mzima. “Kusema
kweli mlitupokea vizuri sana tulipokuja Dar es Salaam na hatuna malalamiko
yoyote yale. Hata hivyo, huu ndiyo uwezo wetu na hatuna la
kufanya.
Hata
Ferroviaro ya Msumbiji walikaa hapahapa walipokuja hapa, alisema Hamdy Ibn
Hossein,” mwakilishi wa Shendi. Rage alisema Simba itacheza mechi yake dhidi ya
Shendi wakati tayari ikiwa imewasilisha malalamiko yake CAF kupitia kwa kamisaa
wa pambano hilo ambaye alitarajiwa kuwasili hapa jana jioni
(Ijumaa).
“Hawawezi
kusema kwamba kwa sababu Ferroviarro walikaa hapa basi na sasa tukae. Hii si
hoteli inayosemwa na CAF, hii ni hosteli ya kuweka wanafunzi. Huu ni uvunjaji wa
wazi wa kanuni na tunaukataa,” alisema.
Ingawa Simba
iliwasili Shendi saa mbili usiku, chakula kilicheleweshwa hadi saa sita usiku
ambako wachezaji waliamshwa kula jambo linaloonyesha kuwa hujuma
zimepangwa.
Jana, magazeti ya
Tanzania yaliripoti kuhusu Simba ilivyotelekezwa katika hoteli ya Safiga jijini
Khartoum kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni bila ya taarifa yoyote huku
wenyeji wakidai wamekwama kwenye foleni.
Kutokana na Simba
kuingia Shendi usiku, Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, aliamua kuwapa wachezaji
mapumziko hadi jana lakini wachezaji waliamua kujifanyia mazoezi
wenyewe.
Mmoja wa wachezaji
waliokuwa wakijifanyia mazoezi binafsi ambayo yanajulikana kwa jina la
individual, alikuwa ni Haruna Moshi Boban ambaye alikutwa akifanya mazoezi ya
peke yake kuzunguka eneo la hosteli ilikofikia timu.
“Tangu juzi
hatujafanya mazoezi kwa sababu ya safari na vituko vya hawa wenyeji wetu.
Nimeamua kujifua mwenyewe kwa sababu ukikaa muda mrefu bila mazoezi hata mwili
nao unazoea ulegevu. Ndiyo maana najifua,” alisema.
Zaidi ya Boban,
wachezaji wengine waliokutwa wakifanya mazoezi majira hayo ya saa tano usiku ni
Mwinyi Kazimoto, Juma Kaseja, Patrick Mafisango, Shomari Kapombe, Uhuru Selemani
na Emmanuel Okwi.
Katika mechi ya
kwanza iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0
na inahitaji sare ya aina yoyote au kufungwa chini ya mabao 3-0 ili kusonga
mbele.
Wakati Simba
wakifanyiwa hivyo, mashabiki wa klabu ya Al
Merreikh ya Sudan wameufanyia fujo msafara wa klabu ya Tout Puissant Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Khartoum, wakidai na wao walipokewa
vibaya na klabu hiyo mjini Lubumbashi wiki mbili zilikzopita.
Mazembe
yenye washambuliaji wawili Watanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel
Ulimwengu ipo Khartoum kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa
Afrika dhidi ya Merreikh, hatua ya 16 Bora.
Katika
vurugu hizo, basi walilokuwa wamepanda wachezaji wa Mazembe limevunjwa vioo na
athari zaidi ikiwemo hali hali za wachezaji bado
hazijajulikana.
Sasa
mechi hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Omdurman, hatima yake ipo
mikononi mwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF)- ambayo inatarajiwa kuchukua hatua
muda mfupi ujao, kubwa zaidi ikitarajiwa kuifuta mashindanoni Merreikh na
kuifungia hivyo Mazembe kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment