Waheshimiwa
Wananchi wenzangu,
Amani
iwe kwenu,
Kwa
kipindi cha wiki nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya
habari, mitandao ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali
kwa mwaka wa fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa
bungeni juu ya udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa
bajeti pamoja na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha,
kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na
Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila
marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa
kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa udhaifu wa
kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi,
udhaifu wa Rais una athiri maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Katika
mazingira haya, udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya
wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa
kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia
migomo baridi ya watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana
pia na madai yao ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni
Uhuru!.
Kadhalika
udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu
wa kanuni 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu
mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote
haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya
serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Pia,
katiba imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti
ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja
bunge suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na
kuwafanya wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu
wa bunge unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika
kuvunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge
kupendekeza mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa
kubadilisha na wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya
udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa
sana kwa nchi na maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa
mantiki hiyo, katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni
ya kuwezesha ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato
wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Wakati katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika
katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa
kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107
ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu
wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika
muktadha huo, nimeanza kufanya uchambuzi
ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni
Uhuru!.
Hata
hivyo, hata kwa kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na
maamuzi ya kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano
Kanuni ya 94 inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara
ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa
mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa
unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni ambayo
toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja pamoja na
kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Mwaka
huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka
wa Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni
2012 hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa
ukamilfu mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru
kwamba Spika wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba
kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo
inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge
kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha
serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na
pendekezo hilo kurudiwa tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012.
Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe
kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa
imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa
nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha
kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia
sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo
hilo lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa
kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais
mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa
mapato kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni
pamoja na kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni
Uhuru!.
Hivyo,
Kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni
yake, ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne
wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya
marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli ni
Uhuru!.
Aidha,
ili kuondoa udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge
(Hansard) za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri
kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10)
kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au
mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa
zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi
kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe
kuwa nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema
bungeni na nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye;
baada ya kujipa muda wa kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati
bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012
na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha
2012/2013; ambapo pamoja na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa
kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali.
Ukweli ni Uhuru!.
Kwa
sasa niwashukuru wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na
watanzania kwa ujumla walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye
mitandao ya kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru
pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali
walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia
uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru
pia kwa mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya
udhaifu wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine
wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili
kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa heshima kwa
wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’.
Ukweli ni Uhuru!.
Wakati
mjadala huu ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu
wa tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya
ofisi ya Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango
wangu wa tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na
umri, naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari
na kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka
zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja
uliopita. Ukweli ni uhuru!.
Niliamini,
naamini na nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio
kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa
kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na
kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job
Ndugai bungeni wa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa;
nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge
utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.
Katiba
ya Nchi ambayo niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara
ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha
Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi
kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote
katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa
mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini,
asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu
udhaifu wa Rais na kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa
uthabiti serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
yanayolikabili taifa; niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa
ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia
serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Tarehe
19 Juni 2012 nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na
tarehe 22 Juni 2012 nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka
misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila
mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa
kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya
miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la
Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na kuingizwa
kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya
maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013. Ukweli ni
Uhuru!.
Pamoja
na utetezi uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya
kiingereza na Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti
kwa kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao
ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia
fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo
kama zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.
Naamini
Rais Kikwete anayofursa ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake
katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha
Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya
matumizi ya nyongeza ya fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha
fedha za maendeleo. Kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam,
serikali kwenye bajeti ya nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za
miradi ya Maji kwa upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi
wa Bwawa la Kidunda, kwa upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango
cha lami kwa barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza
msongamano wa magari, na fidia ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe
wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la
Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa
Wasemaji wa CCM waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na
mwenyekiti wa chama chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha
mmoja wa waasisi wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere ambapo wakati huo taifa likiwa katika
mtanziko alimueleza Rais wa wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa
wa 50 na kuendelea kusema katika Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya
minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa
anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu
wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama” . Ukweli ni Uhuru!
Naamini
Mwalimu Nyerere hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni
kumtuhumu pia Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu
uliojitokeza ni kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake
kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa
serikali na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni
Uhuru!.
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya
mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na woga;
woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo
anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa
tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa
hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa
yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila
binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo
tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama
maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na
wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila
kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa
kunukuu: Ukweli ni uhuru.
Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika
22
Juni 2012
Bungeni-Dodoma
No comments:
Post a Comment