kabesejr blog

kabesejr

albino

Sunday, April 8

Chadema kutikisa Arusha

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo kinatarajiwa kuuteka tena Mji wa Arusha, pale kitakapokuwa na mkutano mkubwa katika Viwanja wa NMC kutoa tamko la ama kukata rufani ya kupinga Mbunge wake, Godbless Lema kuvuliwa ubunge au la.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba alisema jana kwamba Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa wanatarajiwa kuhutubia.

Polisi mkoani Arusha jana walitoa kibali cha kufanyika kwa mkutano huo huku Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa akisema wamekitoa kwa masharti… “Ni kweli tumewapa kibali ila tumewaomba wafuate taratibu za mikutano, wasivunje sheria kwa matamko yao, wamalize saa 12:00 jioni na wasiwe na maandamano.”

Dk Slaa aombwa kugombea
Baadhi ya wananchi na makada wa Chadema wamemtaka Dk Slaa kugombea ubunge wa jimbo hilo ili kuhakikisha kwamba inalitetea.
Mmoja wa makada hao, Julius Minja alisema wakati Dk Slaa anagombea aliyekuwa mbunge, Godbless Lema akate rufani ya kupinga kuzuiwa kugombea kwa miaka mitano ili mwaka 2015 arejee kugombea tena.
“Tunajua walikuwa hawampendi Lema kutokana na harakati zake za kutetea haki za wanyonge. Tuna imani atarudi bungeni tena ila kwa sasa ili tusikae bila mbunge, Dk Slaa tunamuomba agombee," alisema Minja.
Mwanachama mwingine, Happynes Kanangira alisema wana uhakika wa ushindi katika jimbo hilo kwa yoyote ambaye atagombea lakini wanaamini chaguo sahihi kwa sasa ni Dk Slaa.
Hukumu kuvuja
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Herbet na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye wamekana madai ya kuvuja kwa hukumu ya kutenguliwa matokeo ya ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kabla ya kusomwa mahakamani juzi.
Walisema hayo walipohojiwa na mwandishi wetu baada ya kuwepo kwa uvumi kwamba ulinzi ulioimarishwa mahakamani hapo siku ya kesi uliashiria kuwa walijua kwamba Lema atavuliwa wadhifa huo hivyo kuwa tayari kuzima vurugu.
Lema na viongozi wa Chadema akiwepo Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe walidai kupata taarifa za uamuzi wa kesi hiyo hata kabla haijasomwa mahakamani.
“Mimi ninachojua ni kuwa hukumu imesomwa jana (juzi), sasa kusema ilivuja si kweli,” alisema Herbert akitetea hukumu iliyosomwa na Jaji Gabriel Rwakibarila.
Naye Kamanda Andengenye alisema hakuwahi kupata uamuzi wa kesi hiyo kabla ya juzi iliposomwa mahakamani. Akizungumzia kitendo cha kuimarisha ulinzi katika jiji la Arusha kabla ya hukumu hiyo, Kamanda Andengenye alisema ilikuwa ni jambo la kawaida kwa polisi kujiandaa kwa lolote ambalo lingetokea.
“Ulinzi wetu haukumaanisha tulijua matokeo ya kesi, sisi tulijiandaa kwa lolote kwani hata kama matokeo yasingekuwa hivyo, kulikuwa pia na uwezekano wa Chadema kusherehekea kupita kiasi na hivyo polisi wangepaswa kusimamia hilo," alisema Andengenye.
Akizungumzia kuwepo ulinzi hadi Ofisi za Mbunge, alisema haikuwa makosa: “Tulijipanga kuimarisha ulinzi kwa lolote ambalo lingetokea lakini kwa bahati nzuri hali ilikuwa shwari na hakuna ambaye tunamshikilia kwa vurugu zozote ambazo zinahusiana na kesi hiyo.”
Lema alidai kuwa baadhi ya maofisa wa Serikali, wabunge na viongozi wa CCM walimweleza kabla ya kesi hiyo kuwa matokeo ya ubunge wake yalikuwa yanakwenda kutenguliwa.
Mbowe alidai kuwa alipata taarifa mapema na akaonya vyombo vyenye mamlaka ya kutoa uamuzi kusoma alama za nyakati kwani kama vikikubali kuingiliwa kinyume cha taratibu, nchi itaingia katika machafuko.
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilifikia kutoa hukumu hiyo baada ya kesi iliyofunguliwa na wanachama wa CCM Mussa Mkanga (55), Agnes Mollel (44) na Happy Kivuyo (49 ), ambao walikuwa wanamtuhumu Lema kwa kutoa kauli za udhalilishaji, matusi na kashfa kwa aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Dk Batilda Buriani.

Wapinga hukumu
Mawakili kadhaa wamepinga baadhi ya vifungu vilivyotumika katika hukumu. Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC), Kanda ya Arusha, Shilinde Ngalula alisema Jaji Rwakibarila hakukamilisha amri katika uamuzi wake na kuacha baadhi ya mambo yakielea.
Shilinde alisema baada ya kumtia hatiani Lema kwa kutumia Kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi, Jaji alipaswa kwenda mbali zaidi kwa kutamka adhabu zote zinazoambatana na makosa hayo badala ya kutangaza kutengua matokeo pekee.
Alisema anayetiwa hatiani kwa mujibu wa kifungu hicho anakabiliwa na adhabu ya kupigwa marufuku kushiriki shughuli za kisiasa kwa kipindi kisichozidi miaka mitano, lakini katika hukumu yake aliyosoma juzi, Jaji Rwakibarila hakutamka hivyo.
Shilinde ambaye ni Wakili wa Mahakama Kuu alisema kisheria hukumu hiyo ilipaswa kutamka wazi adhabu ya Lema ambayo ni kuvuliwa ubunge na kulipa gharama za kesi pamoja na mambo yote yanayoambatana nayo ikiwemo kuzuiwa kushiriki shughuli za kisiasa kwa miaka mitano kwa kutiwa hatiani kwa makosa yanayoangukia kifungu cha 114.
Kuhusu uwezekano wa kurekebisha mapungufu hayo, Shilinde alisema kisheria, Jaji huyo Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga anaweza kupitia hukumu yake na kurekebisha makosa hayo kwa kuyagundua mwenyewe, kugutushwa na mtu mwingine, pande husika au mamlaka ya juu yake. Njia nyingine ni kupitiwa na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa au Jaji Mkuu kuitisha faili la shauri husika na kuifanyia marejeo na kutoa maelekezo stahili.
Bila kutaka kuizingumzia kwa undani hukumu hiyo, Shilinde alionyesha shaka juu ya kosa la kashfa alilosema ili ithibitike ni lazima maneno yaliyotamkwa yadhihirike kuwa ya uongo kwa sababu iwapo yaliyotamkwa yana ukweli, haiwezi kuwa kashfa.
Alisema kama Lema alitamka maneno hayo na kudhihirika kweli kuwa yalikuwa ya kashfa, basi shauri la kukashifiwa lingefunguliwa na Dk Burian mwenyewe aliyekashifiwa na si mtu mwingine.
“Kesi ya kashfa haiwezi kufunguliwa na mtu mwingine isipokuwa yule aliyekashifiwa. Shauri la kashfa haliwezi kuwa na uwakilishi ndiyo maana ikitokea mlalamikaji katika kesi ya kashfa anafariki dunia, basi shauri lenyewe nalo huishia hapo kwa sababu haliwezi kurithiwa,” alisema.
Dk Burian aliyedaiwa kukashifiwa na Lema hakufungua kesi wala hakufika mahakamani kutoa ushahidi kuhusu madai hayo licha ya Jaji Rwakibarila kusisitiza umuhimu wa ushahidi wake kutokana na kutajwa na mashahidi wote 14 wa upande wa wadai walioitwa mbele yake.
Kwa upande wake, Wakili Method Kimomogoro aliyemwakilisha Lema katika kesi hiyo naye alielezea kusikitishwa na hukumu ya Jaji Rwakibarila aliyodai haikuzingatia hoja zaidi ya 30 alizoainisha kwenye hati yake ya majumuisho.
Alitaja hoja ambazo Jaji hakuzizungumzia wala kuzitolea uamuzi kuwa ni pamoja na wadai kushindwa bila kutoa sababu kuwasilisha nakala za CD zinazomwonyesha Lema akihutubia na kutoa maneno ya kashfa, udhalilishaji na ubaguzi kidini na kijinsia walizodai kuwa nazo.
Kimomogoro alisema Jaji pia alitumia ushahidi wa wadai na mashahidi waliodhihirika kuwa viongozi na wanachama wa CCM, lakini akapuuza ushahidi wa upande wa utetezi kwa madai kuwa mashahidi walikuwa viongozi na wanachama wa Chadema hivyo walikuwa na maslahi.
Alitaja hoja ambayo Jaji hakuishughulikia kuwa ni ushahidi wa kimazingira ulioonyesha kuwa Lema asingetoa maneno aliyodaiwa kusema kuhusu ya uwezo kiungozi dhidi ya wanawake kwa sababu kwenye timu yake ya kampeni alikuwa akiongozana na wagombea udiwani wanawake ambao aliwanadi kwa wapiga kura na pia Chadema ilisimamisha mgombea ubunge mwanamke katika Jimbo la Longido ambalo wenyeji wake ni Wamasai.
Alisema hata Dk Burian aliyedaiwa kukashifiwa, hakuwahi kulalamika kwenye Kamati ya Maadili ya Jimbo wala CCM hakikuwahi kulalamika licha ya kupewa fursa hiyo kisheria.
Alisema kwa kuacha hoja nyingi bila kuzishughulikia na kuzitolea uamuzi, ndiyo maana Jaji aliweza kusoma na kumaliza hukumu yake ndani ya saa moja.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...