MAWAZIRI WATIBUANA NI NUNDU NA MFUTAKAMBA
WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu amesema anapigwa vita na Naibu Waziri wake, Athumani
Mfutakamba baada ya yeye kupinga Kampuni ya CCCC kupewa zabuni ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Nundu alisema
CCCC iliwahi kwenda kumshawishi yeye ili akazungukie katika nchi
mbalimbali kutembelea miradi ya kampuni hiyo, lakini alikataa kwa vile
alijua kuwa kufanya hivyo ni kama hongo.
Nundu alisema lakini cha ajabu, Naibu Waziri wake alipofuatwa na
kampuni hiyo, alikubali na akapelekwa kwenye nchi za Mauritius, China na
Guinea Bissau bila hata kumtaarifu bosi wake.
Alisema uhusiano wake na Naibu Waziri ulianza kuingia dosari wakati
wa ujenzi la jengo la maegesho katika Bandari ya Dar es Salaam ambalo
Nundu aliusimamisha baada ya kuona zabuni ya ujenzi wake hauna mashiko.
Aidha, Nundu alidai Mfutakamba aliwahi kumsemea yeye kwa Rais Jakaya
Kikwete wakati alipotembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuwa
anazuia mradi huo.
“Nashukuru Mungu Rais alikuwa ameshapata taarifa ubabaishaji uliopo kwenye mradi
huo naye akaomba ujenzi wake usitishwe kwanza,” alisema Waziri huyo.
Alisema amekuwa mstari wa mbele kupinga miradi yote yenye dalili za
rushwa, lakini baadhi ya watendaji ndani ya taasisi zilizoko chini ya
wizara yake, wanamshutumu kuwa anaingilia maslahi ya mashirika hayo.
“Mimi ni kama mtu yuko porini na amevamiwa na majambazi anapiga
kelele, lakini hakuna mtu wa kumsaidia,” alisema Nundu akimaanisha kuwa
wanaompiga vita ni wale ambao wanataka kufuja fedha kwa kutumia miradi
ambayo yeye anaona kuna mianya ya rushwa.
Kutokana na hali hiyo, Nundu asisitiza kuwa haoni sababu ya yeye
kujiuzulu kwa kuwa hana kosa lolote alilolifanya na jambo analolitetea
ni kwa maslahi ya nchi yake.
Alisema hana njaa ya kuiba fedha za umma, kwani kwa nafasi ambazo
amewahi kushika tangu awe mtumishi sehemu mbalimbali nchini na nje ya
nchi, ana fedha za kutosha za kuishi vizuri yeye na familia yake.
Alisema ana machungu na taifa lake na anafanya kazi ya uwaziri kama
kulipa fadhila kwa taifa ambalo lilimsomesha ndio maana anapigwa vita
kila kona, kwa sababu amebana ulaji wa baadhi ya watu ndani ya wizara
yake na ndani ya TPA.
Nundu alisema sio kwamba yuko kwenye nafasi ya uwaziri kwa ajili ya
kusaka fedha, bali anataka kulisaidia taifa lake na amekuwa anajitahidi
kufanya kazi kwa maadili makubwa.
Mbunge huyo wa Tanga Mjini, ni miongoni mawaziri ambao inadaiwa
ameshinikizwa ajiuzulu kutokana na wizara yake kufanya madudu, likiwemo
suala la kuingilia utendaji wa Menejimenti ya TPA.
Lakini Nundu katika maelezo yake ya jana, alisisitiza kuwa hakuwahi kuingilia utendaji wa TPA,
bali anachotaka yeye ni ujenzi wa gati namba 13 na 14 upate
mwekezaji ambaye amefuata taratibu na gharama zake ziwe zimehakikiwa na
Serikali.
Alisema kitendo cha Menejimenti ya TPA kumtafuta mwekezaji bila kushindanishwa ni ukiukwaji wa taratibu za Serikali.
Alisema kuna kampuni zipatazo 12 ziko tayari kujenga gati hiyo.
Alisema anataka kila kampuni ipewe fursa ya kufanya upembuzi yakinifu
waone ni kampuni gani yenye gharama nafuu.
Kwa upande wake, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu madai ya bosi wake,
alisema safari alizosafiri kwenda nchini China, Guinea na Mauritius
aliondoka wakati waziri huyo akiwa safari ndio maana hakumwaga.
Lakini alisema alifuata taratibu zote za kiserikali kwani alimwaga Waziri Mkuu na akapewa ruhusa.
Alisema nia yake ya kwenda kutembelea miradi ya kampuni ya CCCC ni
kutaka kuona uwezo wa kampuni hiyo badala ya kuwapa mradi huo wa ujenzi
wa upanuzi wa bandari bila kujiridhisha.
“Kweli nilienda China ambako niliona wanajenga reli, wanaongeza kina
cha bahari na wanajenga magati katika miradi yao hiyo,” alisema naibu
waziri huyo na kukanusha kuondoka bila kumwaga bosi wake huyo kuwa
hawezi kufanya hivyo kwa kuwa anafahamu taratibu za
kazi.
Alisisitiza kuwa baada ya kurudi nchini, aliandika ripoti nzuri na
kuiwasilisha kwa bosi wake na kwa Waziri Mkuu kuhusu alichokiona kwa
wawekezaji wa CCCC ambao wameomba kupanua bandari ya Dar es Salaam.
Alisema katika miradi yote inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya
wizara hiyo, amekuwa anamshauri bosi wake kwa maandishi njia nzuri ya
kushughulikia miradi hiyo na kufanya hivyo sio kwamba anampiga vita.
“Mimi ndiye mshauri wake mkuu nilichomweleza kuhusu TPA niliweka wazi kuwa lile ni shirika
linaloruhusiwa kisheria kufanya manunuzi yake,” alisema na kuongeza
kuwa alimshauri vile kwa kutambua kuwa TPA ina Bodi ambayo inajua namna
nzuri ya kuwapata wawekezaji kuliko wizara ikiingilia.
Alisema alimshauri pia kuwa kazi ya wizara ni kuandaa sera, miongozo na taratibu za namna ya kumpata mwekezaji.
“Nimekuwa mkuu wa wilaya kwa miaka mitano, nafahamu taratibu za
kiserikali za kuondoka nje ya nchi na majukumu ya wizara,” alisema
Mfutakamba ambaye kabla ya kuwania ubunge na kushinda Jimbo la Igalula
mkoani Tabora, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani
Iringa.
Akizungumzia juu ya ushauri alioutoa kuhusu upanuzi wa TPA,
Mfutakamba alisoma barua aliyoiandika alishauri iwepo mipaka ya
kimajukumu kati ya TPA na wizara katika utekelezaji wa mradi huo wa
ujenzi wa gati namba 13 na 14.
Alisema alifafanua pia kuwa jukumu la kumlipa mwekezaji ni la TPA
hivyo ni vyema mamlaka hiyo kupitia Bodi yake ikaweka vigezo wanavyoona
vinafaa katika kumpata mwekezaji na lengo ni kumpatia mwekezaji ambaye
atalipa taifa faida.
“Hayo ndio naweza kusema, maana nafahamu kushauri sio kumpiga vita mtu,” alisema naibu
waziri huyo na kuongeza kuwa ni vyema sasa kile ambacho kimeazimiwa
na Bunge kiachwe kifanye kazi kwa Serikali kujiridhisha katika kufanya
tathmini ya gharama halisi za ujenzi wa mradi huo.
Kampuni ya CCCC katika upembuzi yakinifu ilioufanya imebainisha
gharama za ujenzi wa gati hilo kuwa ni Dola za Marekani milioni 540,
lakini Nundu anadai kuwa kati ya kampuni 12, kampuni mbili zimekubali
kujenga gati hilo kwa Dola za Marekani milioni 300
No comments:
Post a Comment