Siku saba baada ya takwimu za shuti moja bao moja
kwa Chelsea na mashuti zaidi ya 24 bila mabao kwa Barcelona kwenye uwanja wa
Stamford Bridge, timu hizi zinarudiana
kwenye uwanja wa Nou Camp.
Barcelona wamekuwa kwenye wakati mgumu baada ya
kufungwa mechi mbili mfululizo huku nyota wake Lionel Messi akisindwa kung'aa
kwenye kwenye mechi zote mbili.
Chelsea walipoifunga Barca mapema wiki iliyopita
wengi waliona kuwa timu hii toka London imepanda baiskeli ya miti na Barcelona
ingeshinda kiwepesi mchezo wa marudiano . Hata hivyo kipigo cha kwenye El
Classico kimewaweka Barca kwenye hali tofauti ya kisaikolojia ambayo inaweza
kuwa sababu ya aidha kushinda au kufungwa kwenye mchezo wa
marudiano.
Ukirudi nyuma na kutazama sababu ambazo zinaweza
kuwa zimeipelekea Barca kufungwa michezo yote miwili na kuzichanganya kwa pamoja
hapa ndio unapoweza kugundua hali ngumu waliyo nayo Barca hii
leo.
Kwenye mechi ya jumatano iliyopita mfumo waliotumia
Chelsea na bahati kwa pamoja viliwasaidia vijana wa Di Matteo. Mfumo aliotumia
siku hiyo ulikuwa rahisi,kuta mbili za wachezaji wanne kila moja nyuma ya mpira
na kujaribu kupunguza nafasi ya Barca kufaidi kumiliki mpira kuanzia katikati
mwa uwanja kuelekea liliko lango la Chelsea .
Pamoja na
hilo , Di Matteo aliwaelekeza viungo Raul Meireles na John Obi Mikel kuhakikisha
wanakufa na Lionel Messi ,Xavi na Andres Iniesta huku Ramires akifanya kazi ya
kuua mashambulizi ya upande wa kulia aliko Mbrazil mwenzie Dani Alves . Mbinu
hizi zilifaulu kwa kusaidiwa na ari waliyokuwa nayo Chelsea kisaikolojia pamoja
na bahati iliyokuwa upande wao kwani ukiachilia mbali jinsi Chelsea
walivyoshinda huwezi kusahau mara ambazo Barca waligongesha miamba na mara
ambazo Petr Cech alifanya kazi ya ziada kuokoa au mabeki kina Ashley Cole
wakiondosha hatari langoni mwao.
Kwenye mchezo dhidi ya Real, Barca waligharimiwa
sana na kuwakosa wachezaji mbadala wanaoweza kufanya kazi ya ufungaji zaidi ya
Lionel Messi. huwezi kuacha kufikiri kuwa nafasi mbili alizopata Christian Tello
na kushindwa kuzitumia zingekuwa zimetumiwa vyema na mtu kama Pedro au David
Villa .
Pengo la David Villa limeonekana sana kwenye El
Classico na kuna kila uwezekano kuwa endapo Chelsea watafuzu basi pengo hilo
litaonekana kwenye mchezo huo pia. Pamoja na hayo Real walikuwa na aina ya
uzoefu na uwezi wa kutumia nafasi chache za kufunga walizozipata jambo ambalo si
timu nyingi zinazocheza na Barca zinafanya.
Ukiwaangalia Barcelona wenyewe kama Barcelona kuna
baadhi ya viashiria mbalimbali ambavyo vilionyesha kuwa hawako mchezoni siku ya
jumamosi. Lionel Messi hana kawaida ya kuwa mlalamishi lakini alilalama kwa
waamuzi kuliko mchezaji yoyote siku ile na hata Xavi na wengineo walikuwa
wanaonekana kupagawa jambo ambalo linakufanya uhisi kuwa ile hali ya woga ambayo
timu pinzani inakuwa nazo ikicheza dhidi ya Barca inakuwa nayo imehamia kwa
Barcelona wenyewe.
Safu ya ulinzi nayo imekuwa tatizo kubwa. Carles
Puyol anastahili kubeba lawama kwenye
mabao yote matatu ambayo Barca imeruhusu kwenye michezo miwili iliyopita na
endapo atacheza tena huenda Di Matteo akawaelekeza wachezaji wake kupeleka
presha kwenye upande wake .
Hata hivyo Barcelona wanabaki kuwa timu yenye uwezo
hata pale ambapo wanapitia kwenye kipindi kigumu kama livyokuwa kwenye msimu huu
na quality yao pekee ambayo dhahiri shahiri ni bora kuliko ya Chelsea inaweza
kutosha kugeuza matokeo.
Kikubwa kitakachoamua mchezo ni hali ya
kisaikolojia ya wahezaji a Barcelona.
Wanapaswa kuacha yaliyotokea kubaki huko nyuma
yaliko na ku-deal na mchezo wa leo kama wa leo . Endapo wataruhusu kuingiwa na
hali ya woga kwa maana wanaweza kufungika kirahisi. Kwa hali ya kawaida Barcelona ni washindi na hiki ni kitu ambacho
wahezaji wanaingia nacho uwanjani kwa kuwa wana "winning mentality" . Ila hiyo
hiyo mentality inaweza kuondoka na swali ambalo kila mmoja anajiuliza ni kama
hiyo winning mentality ipo baada ya michezo miwili migumu ambayo Blaugurana
wamefungwa?
Chelsea wana nafasi finyu ya kupata ushindi kwenye
mchezo wa leo na nafasi pekee kubwa waliyo nayo ya kusonga mbele ni kutafuta bao
la ugenini huku wakilinda kwa nidhamu kama waliyolinda nyo kwenye mchezo wa
Stamford Bridge .
Tetesi toka kwenye magazeti ya Hispania kwa masaa
24 yaliyopita zimekuwa zikisema kuwa Lionel Messi hayuko kwenye physique nzuri ,
pengine michezo imekuwa mingi mfululizo pengine kama ilivyo kwa kila binadamu
wachezaji wa Barcelona wamechoka baada ya kuwa na msimu ambao mambo yamekuwa
magumu kwao ?
Haya ni maswali ambayo majibu yake yatapatikana
ndani ya masaa machache yajayo
No comments:
Post a Comment