ISHARA ZA KIFO CHA KANUMBA
KUNA wakati binadamu anafanya kitu kwa kutumwa na nafsi yake bila kujua kinachokuja mbele. Pia kuna uhusiano mkubwa kati ya matendo ya mtu ambayo huashiria jambo linalofuata maishani mwake. Kwa ufupi ni kujitabiria.
Kabla ya kukutwa na umauti usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu, aliyekuwa mwigizaji mkubwa Bongo, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ (28), kulikuwa na ishara zilizoashiria kifo chake.
YEYE NA MZEE KIPARA
Ishara ya kwanza iliyoashiria jambo fulani ilikuwa hivi; kabla ya aliyekuwa mwigizaji mkongwe, marehemu Fundi Said ‘Mzee Kipara’ kutangulia mbele za haki Januari 11, 2012, marehemu Kanumba na baadhi ya waigizaji walimtembelea maeneo ya Kigogo, Dar akiwa mgonjwa wa miguu ambapo alisalimiana nao kwa furaha isipokuwa maremu Kanumba.
Alipomshika marehemu Kanumba mkono, alimtazama usoni kisha akaanza kulia jambo lililowashtua wasanii wenzake ilihali wakijua kuwa alikuwa akimpenda Kanumba kupita maelezo. Kwa sasa watakuwa wamekutana huko ahera!
WIMBO WAKE
Wimbo aliouimba wa Nitanyanyua Macho, una maneno yaliyoashiria kifo hasa pale anaposema, ‘msanii maarufu ameaga dunia, pengo la Kanumba halitazibika, hata wanaonichukia watabeba jeneza langu’.
Maneno hayo yalitosha kabisa kuthibitisha kuwa nafsi yake ilijua jambo linalokuja mbele bila yeye kujijua.
AWA MPOLE GHAFLA
Usiku wa kuamkia Ijumaa ya Aprili 6, mwaka huu, Kanumba alikuwa ndani ya Ukumbi wa New Maisha, Masaki, Dar, tofauti na alivyozoeleka, alikuwa mpole kupita maelezo.
Ukweli ni kwamba hata wewe ungemuona, ungejua kuna kitu kwani muda wote alikuwa kaweka mikono shavuni na wala hakujiachia na burudani ya muziki kama siku nyingine.
KUZUSHIWA KIFO
Kabla ya kufikwa na umauti, marehemu Kanumba aliyezaliwa Januari 8, 1984, alishazushiwa kifo mara mbili. Mara ya kwanza alilalamikia mitandao ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuandika kuwa amekufa huku akidunda Bongo.
Pia, hivi karibuni ilisambazwa meseji ya kizushi kuwa amepata ajali na kufariki dunia akiwa Mbeya ambapo alikiri kupata usumbufu huku akijitahidi kukanusha uvumi huo.
WIMBO KABLA YA KULALA
Kwa mujibu wa mdogo wake aliyekuwa akiishi naye nyumbani kwake pale Vatican-City, Sinza jijini Dar, Seth Bosco, wakati wa chakula cha jioni, marehemu Kanumba alichukua gitaa lake na kuwaburudisha watu kwa wimbo uliobeba maudhui ya kupendana akiwasisitiza kuwa upendo ni jambo muhimu katika maisha. Bosco aliyaelezea maneno hayo kuwa ilikuwa ni ishara ya kuwaaga.
MANENO YA MWISHO MTANDAONI
Kupitia ‘blogu’ yake, marehemu Kanumba aliyewika ndani na nje ya Bongo alisisitiza umuhimu wa kusaidia jamii ambapo aliwaasa binadamu kusaidia wenzao.
Aliandika: “Kusema kweli linapokuja jambo la kusaidia jamii najitahidi kutoa ninachokuwa nacho maana hapa nakumbuka maneno ya Mwandishi Albert Pine…”What we do for ourselves dies with us. What we do for others and the world remains and is immortal.”
Rest In Peace (R.I.P) The Great!
No comments:
Post a Comment