MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga amejibu
mapigo ya Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka kuichukua timu kufuatia
mgogoro unaoendelea klabuni.
Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa
Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb,
wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari
kuachia ngazi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya
leo, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es
Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha
jana imekubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
Aidha, kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli
alifanya nao kikao ana akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa
mujibu wa Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha
ili ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa
watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye
matatizo.
Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya
mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi
madaraka ya uongozi.
Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya
Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wao watahudumia timu, lakini mapato ya mechi
watachukua akina Nchunga.
Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa Yanga
walipewa mapumziko na jana walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa
walikwama kwa sababu ya mvua.
Mwenyekiti wa Yanga, Nchunga amesema timu sasa itaingia
kambini kesho na kuanza mazoezi moja kwa moja chini ya makocha Fred Felix Minziro
na Salvatory Edward, wakati huo akisikilizia Wazee kama watatekeleza masharti
yake awakabidhi timu.
SOURCE: (bongostaz.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment