YANGA YAICHARAZA POLISI DODOMA JANA
TIMU ya soka ya Yanga jana iliwapooza machungu mashabiki wake kwa kuifunga timu ya
Polisi Dodoma mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jana.
Yanga ambayo ilipoteza mechi mbili mfululizo kwa kufungwa mabao 3-2 na ndugu zake Toto
Africans ya Mwanza na kisha kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa
Kagera Sugar kwenye mechi hizo za Kanda ya Ziwa, iliwachukua dakika 18
kuandika bao la kwanza lililofungwa
na mshambuliaji Davis Mwape aliyepata pasi ya Hamisi Kiiza.
Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa beki wa kushoto wa timu hiyo
Oscar Joshua aliyepiga shuti kali akiwa nje ya 18 na kumgonga beki mmoja
wa Polisi Dodoma na mpira ukamkuta Hamisi Kiiza aliyemtengea Mwape
akiwa ndani ya eneo la penalti aliyefunga kwa urahisi.
Yanga ilipata bao la pili dakika ya 54 lililofungwa na winga wa
kushoto wa timu hiyo Idrissa Rashidi baada ya kupokea pasi nzuri ya
Haruna Niyonzima aliyegongeana vyema na Rashidi Gumbo aliyeng’ara kwenye
mechi hiyo.
Yanga iliandika bao la tatu dakika ya 60 lililofungwa na Mwape aliyefunga kwa shuti kali.
Kwenye mechi hiyo iliyoshuhudiwa na watazamaji wachache Polisi
walipata bao lao mfungaji akiwa Ismaili Mkama kwa shuti kali dakika ya
76.
Kutokana na matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 46 na kufufua
matumaini ya kucheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwakani
kama Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania
Bara itapoteza michezo yake iliyobaki.
Azam ina pointi 50 na leo inacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam
Chamazi, ambapo kama Azam itashinda itafikisha pointi 53, ndoto za Yanga
zitakuwa zimepotea kwani kama Yanga ikishinda michezo yake miwili
iliyobaki itafikisha pointi 52, hivyo Azam itashiriki michuano ya
kimataifa mwakani.
Kama leo Azam itapoteza mchezo wake kwa kufungwa ama kutoka sare,
kisha Simba inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 56 ikaifunga Moro
United inayoshika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 19, Simba
itakuwa imetangazwa bingwa mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa
2011/12.
Simba itafikisha pointi 59 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu
nyingine yoyote kati ya 14 zilizopo kwenye ligi hiyo, kwani timu pekee
yenye uwezo wa kuzifikia ni Azam, ambayo kama
itateleza kwa sare au kufungwa basi ubingwa utakuwa wazi Msimbazi.
No comments:
Post a Comment