kabesejr blog

kabesejr

albino

Sunday, April 15

MCHEZAJI AANGUKA UWANJANI, AFARIKI DUNIA

Wachezaji wenzake wakisikitika
Morosini akiwa amebebwa kwenye machela

Mechi za mwishoni mwa wiki nchini Italia zimefutwa Jumamosi, kufuatia kifo cha kiungo wa klabu ya Livorno, Piermario Morosini uwanjani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa akicheza kwa mkopo kutoka klabu ya Serie A, Udinese, alizimia wakati wa mechi ya Ligi Daraja la Pili huko Pescara na baadaye ikatangazwa amefia hospitali.

Huo ni mfululizo wa majanga kihistoria katika familia yao, kwani hata wazazi wake Morosini walifariki wakati akiwa mdogo, wakati kaka yake pia aliuawa.

Alikuwa anaishi na dada yake tu.

Kifo cha Morosini kinakuja ndani ya mwezi mmoja, baada ya kiungo wa Bolton Wanderers ya England, Fabrice Muamba apatwe matatizo ya moyo na kuzimia uwanjani katika Robo Fainali ya Kombe la FA na Tottenham, ingawa amenusurika baada ya kutibiwa.

Meneja Mkuu wa Shirikisho la Soka Italia, Antonello Valentini alichukua hatua kufuatia tukio hilo kwa kusimamisha mechi zote za wikiendi hii jana, kuanzia mechi ya Serie A kati ya AC Milan na Genoa.

Mechi hiyo ilitarajiwa kuanza saa 3:00 usiku na tayari mashabiki walikuwa wamekwishaingia kwenye Uwanja wa San Siro, ingawa tangazo hilo lilizomewa na watu wengine.

Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Italia, Giovanni Petrucci baadaye alifanya kikao na bodi zote za michezo nchini humo kuagiza kutoa dakika kadhaa za kuomboleza kifo cha Morosini.

Morosini alipatwa na mshituko wa moyo katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kabla ya kuzimia na pamoja na kupatiwa huduma ya kwanza uwanjani, ilibidi achukuliwe na gari la wagonjwa kukimbizwa hospitali ya Civile Santo Spirito, Pescara kwa matibabu zaidi.

Lakini mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia chini ya umri wa miaka 21, baadaye ilitangazwa amefariki dunia.

Lakini Polisi wameshushiwa lawama kwa kifo cha mchezaji huyo kutokana na kuchelewa kuifungulia milango gari ya wagonjwa wakati inaondoka baada ya kumchukua kumuwahisha hospitali.

Mamlaka za Italia zimeanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo, lakini wataalamu wa moyo wamesema ucheleweshaji haujasababisha tofauti.

"Dakika moja mbele au nyuma ndani ya ambulance isingeweza kufanya kitu chochote," alisema Daktari mtaalamu wa moyo, Dk Paloscia.

"Moyo wake ulisimama na mapigo yasingeweza kufanya kazi tena. Tulijaribu kuokoa maisha yake kwa saa nzima na nusu, lakini ilishindikana."

Vyombo vya habari Italia vilishitukia kifo cha Morosini mara baada ya kuanza kusikia vilio kutoka kwa wachezaji wenzake waliokuwa hospitali.

Polisi walianza kuwatawanya Waandishi wa Habari, lakini taarifa rasmi ilifuatia baadaye.

Rais wa FIFA, Sepp Blatter ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Morosini.

Muamba alizimia Machi 17, mwaka huu na akazua hofu kwamba angeingia kwenye orodha ya wanasoka waliofia uwanjani, mtu anayekumbukwa zaidi akiwa ni Marc-Vivien Foe.

Akiwa ana umri wa miaka 28, kiungo huyo wa zamani wa Cameroon aliyezichezea klabu za West Ham United, Manchester City na Lyon, alifariki dunia baada ya kuanguka na kuzimia katika mechi ya Kombe la Mabara Nusu Fainali, dhidi ya Colombia mjini Lyon, Ufaransa Juni mwaka 2003

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...