SHULE YA SEKONDARI KIDELEKO YAUNGUA MOTO
WANAFUNZI
takriban 50 wa Shule ya Sekondari Kidereko wilayani Handeni hawana sehemu ya
kujihifadhi baada ya bweni lao kuteketea kwa moto pamoja na baadhi ya vifaa vyao
vya shule.
Bweni hilo
liliteketea kwa moto hivi karibuni majira ya asubuhi baada ya kutokea kwa
hitilafu ya umeme kwenye bweni hilo muda ambao wanafunzi wote walikuwa
wakiendelea na masomo darasani.
Akizungumza na
Thehabari.com eneo la tukio Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Khamis Said
amesema vitu vyote vya wanafunzi takribani 50 waliokuwa wakiishi katika bweni
hilo viliteketea kwa moto, yakiwemo madaftari ya wanafunzi, nguo, magodoro na
vitanda vya mbao viliteketea kwa moto.
“Hatukufanikiwa
kuokoa kitu maana baada ya kusikika mlipuko na baadhi ya watu kuona moshi
ukitoka ndani ya bweni hilo ambalo muda huo lilikuwa limefungwa tulikuta moto
umesha tanda ndani na ukiwaka kwa kasi jambo hali ambayo ilikuwa ngumu kuokoa,”
alisema Said.
Amesema kwa sasa
wanafunzi hao wanasaidiwa na wanafunzi wenzao kimalazi huku wakiishi kwa shida
kutokana na msongamano uliopo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto. “Unajua
baada ya ajali walibaki na nguo za shule walizokuwa wamevaa siku hiyo pamoja na
madaftari ya vipindi vya siku hiyo tu, vifaa vingine vyote viliteketea kwenye
ajali hiyo…shule imetoa baadhi ya fedha na kuwanunulia maitaji kadhaa japokuwa
hayatoshelezi” alisema Mwalimu Said.
Hata hivyo
alisema tayari uongozi wa idara ya elimu wilaya ya Handeni umetembelea eneo la
tukio na wanafanya utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao. Hii ni mara ya pili
kutokea kwa majanga ya moto shuleni hapo kwani mwaka 2000 wanafunzi walichoma
ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo baada ya kuzuka kwa vurugu kati yao na uongozi wa
shule.
No comments:
Post a Comment